Usawiri wa Ukabila Katika Riwaya Teule za Kufa Kuzikana na Narejea Nyumbani
Abstract
Ukabila unazidi kuongezeka katika jamii na kutishia maisha ya usoni ya mataifa mengi ulimwenguni. Katika utafiti huu, tulishughulikia suala la ukabila na athari zake kwa jamii ya mwanadamu. Riwaya ya Ken Walibora Kufa Kuzikana (2006) pamoja na ile ya Jeff Mandila Narejea Nyumbani (2014) zilirejelewa. Utafiti uliofanywa ulilenga kuafikia malengo matatu mahususi yafuatayo ; kubainisha vichochezi vya ukabila katika jamii namna vinavyojitokeza katika riwaya teule. Pili, kuchanganua athari za ukabila kwa jamii ya mwanadamu na mwisho kutathmini mbinu mwafaka za kukabiliana na ukabila kwa mujibu wa riwaya mbili teule. Utafiti huu ulitumia nadharia mseto ambazo ni ile ya Uyakinifu wa kijamii pamoja na ya Usemezano. Utafiti huu ulikuwa wa maktabani ambapo idadi lengwa ilikuwa matini na makala yaliyo na jumbe kuhusu ukabila. Hata hivyo, kupitia kwa mbinu ya kimaksudi tuliteua riwaya za Kufa Kuzikana na Narejea Nyumbani ili kuchunguza namna watunzi wake walivyoangazia suala la ukabila katika jamii. Vile vile, kule maktabani tulisoma magazeti, majarida, tasnifu za wasomi mbalimbali, vitabu vya ziada pamoja na kupekuapekua mtandao ili kurutubisha data inayohusiana na suala la ukabila katika jamii ya mwanadamu. Uchanganuzi wa data ulifanyika kwa njia ya uchambuzi wa kimaelezo na ufafanuzi. Vichochezi vya ukabila, athari zake katika jamii pamoja na mbinu za kukabiliana na uovu huu vilichambuliwa na kuwasilishwa kuambatana na malengo na mihimili ya nadharia zilizodokezwa. Data iliyozalishwa na utafiti huu itakuwa ya manufaa makubwa kwa jamii inayorudishwa nyuma na suala lililopitwa na wakati la ukabila. Mapendekezo yake yatasaidia jamii kukabiliana na ukabila unaozidi kudidimiza maendeleo ya kiuchumi siku baada ya siku
Fields of Study & Subjects
Postcolonial and Cultural Literary Studies
Literature: history
themes
analysis
Folklore
Mythology
and Literature Studies
Publication details
- Journal / source
- East African Journal of Swahili Studies
- Volume
- 9
- Issue
- 1
- Pages
- 58–78
- Publication date
- 29 January 2026