Tathimini ya Uwiano wa Msamiati kwa Wanafunzi wa Kiwango cha Awali Katika Matini za Kufundishia Kiswahili kwa Wageni

Read full text
Authors: Fatma Fereji Abeid
Cited by: 0

Abstract

Makala hii inatathmini uwiano kati ya msamiati unaotumika katika matini za kufundishia Kiswahili kwa wageni na kiwango cha uelewa cha wanafunzi wa hatua ya awali. Tathimini imefanyika kwa kutumia matini kutoka kitabu cha kufundishia Kiswahili kwa wageni kinachotumika katika Idara ya Kiswahili kwa Wageni, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Lengo kuu la tathimini hiyo ni kubaini iwapo msamiati uliomo kwenye matini hizo unalingana na uwezo wa ujifunzaji wa wanafunzi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ufundishaji wa lugha ya kigeni, hususan vigezo vya A1-A2 vinavyoainishwa katika Mfumo wa Kurejea Lugha Barani Ulaya (CEFR). Uchunguzi huu umetumia mbinu mbili ikijumuisha uchambuzi wa matini na usaili kwa walimu na wanafunzi ili kupata mtazamo wa kitaalamu na wa kiutendaji kuhusu uteuzi na uwasilishaji wa msamiati. Uchambuzi umeongozwa na Nadharia ya Lugha Mfumo-Kazi (Halliday, 1978), ambayo inasisitiza nafasi ya lugha katika muktadha wa matumizi halisi. Matokeo yanaonesha kuwa sehemu kubwa ya msamiati uliojitokeza katika matini ni wa msingi na wa kujirudiarudia, ambao unawiana na mahitaji ya wanafunzi wa kiwango cha awali. Aidha, matumizi ya nomino, vitenzi na vihisishi yameonekana kutawala katika matini, jambo linalorahisisha upokeaji wa lugha kwa wanafunzi wapya. Hata hivyo, baadhi ya changamoto zimebainika, zikiwamo uwepo wa maneno yasiyo ya kiwango cha awali, upungufu wa miundo ya sentensi changamano na makosa ya kisarufi yanayoweza kuathiri uelewa. Uchunguzi unapendekeza marekebisho katika upangaji wa msamiati, uboreshaji wa matini changamano kwa viwango vinavyofuata na kuongeza uhusiano kati ya msamiati na mazingira halisi ya kijamii ya wanafunzi. Kwa ujumla, matini zinaonesha uwiano mzuri lakini unahitaji kuboreshwa ili kuongeza ufanisi wa ujifunzaji.

Fields of Study & Subjects

EFL/ESL Teaching and Learning Linguistic Education and Pedagogy Second Language Learning and Teaching

Publication details

Journal / source
East African Journal of Swahili Studies
Volume
9
Issue
1
Pages
141–152
Publication date
17 February 2026
Language
SW