Uchambuzi wa Miktadha ya Kijamii na Mchango Wake katika Ujifunzaji wa Kiswahili kama Lugha ya Pili Nchini Burundi
Abstract
Makala hii inahusu miktadha ya kijamii na mchango wake katika kujifunza Kiswahili kama lugha ya pili nchini Burundi. Muktadha wa kijamii huathiri ujifunzaji wa lugha ya pili kwa kuchochea mawasiliano ya kuongea, kukuza, na kuboresha matumizi halisi ya lugha katika mazingira ya kawaida (Ellis R., 2008). Hali hii ilimchochea mtafiti kufanya utafiti huu ili kubainisha miktadha ya kijamii iliyopo jijini Bujumbura na kuonesha mchango wake katika kujifunza Kiswahili kama lugha ya pili. Mbinu ya hojaji ilitumiwa kukusanya data. Aidha, mbinu ya usampulishaji tajwa ilitumika kuteua watoataarifa. Watoataarifa hao walikuwa wanafunzi 20 kutoka Chuo Kikuu cha Burundi, kiwango cha shahada ya awali. Nadharia ya Utamaduni Jamii iliyoasisiwa na Mwanasaikolojia Vygotsky (1978) iliongoza utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha kuwa miktadha ya kijamii ya kujifunza Kiswahili jijini Bujumbura ni soko, hospitali, zahanati, nyumbani, na kadhalika. Matokeo pia yalionesha kuwa miktadha hiyo inawawezesha wanafunzi kuingiza msamiati mpya, kukuza stadi za kusikiliza na kuzungumza. Inawawezesha pia, kuimarisha umilisi wa utamaduni na maarifa kuhusu fasihi. Serikali ya Burundi inaombwa kuchukua miktadha ya kijamii kama mikakati rasmi inayochangia kujifunza Kiswahili nchini. Mwisho, makala hii inapendekeza serikali ya Burundi iwezeshe walimu wa Kiswahili kufuatilia ujifunzaji wa Kiswahili wa wanafunzi nje ya darasa.
Fields of Study & Subjects
Linguistic and Sociocultural Studies
Multilingual Education and Policy
Language and Culture
Publication details
- Journal / source
- Eastern Africa Journal of Kiswahili (EAJK)
- Volume
- 5
- Issue
- 1
- Publication date
- 9 February 2026
- Language
- SW